Muwekezaji wa Klabu ya Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’ amefunguka baadhi ya mambo anayotarajia kuyafanya ndani ya klabu hiyo kwa miaka kadhaa ijayo.
‘Mo’ ameweka wazi mipango hiyo, alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Ijumaa (Julai 30) jijini Dar es salaam, wakati akikabidhi Shilingi Bilioni 20 za uwekezaji ndani ya klabu hiyo.
amesema sehemu ya mipango yake ni kuhakikisha Simba SC inakua na viwanja karibia vinane (8), sambamba na uwanja mkubwa ambao utatumika kwa michezo ya Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
“Tuna mipango mikubwa sana huko mbeleni kuwa na viwanja karibia 08, kuwa na uwanja wetu mkubwa na uwekezaji mwingine”
“Lakini pia mipango ya kutetea ubingwa bado ipo na hata kule Afrika ile robo fainali sasa haipendezi, kama kocha wa Al Ahly amesema amefungwa na Bayern Munich na Simba ndizo zilimpa ugumu, basi nami nasema sitaridhika mpaka tupate ubingwa wa Afrika,“ amesema Mo Dewji.
Simba SC imemaliza Msimu wa 2020/21 kwa mafanikio makubwa ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo na Kombe la Shirikisho (ASFC) mara mbili mfululizo, huku ikiishia hatua ya Robo Fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.