Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’ mapema leo Ijumaa (Julai 22) amempongeza Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pape Osmane Sakho kwa kutangazwa kuwa mshindi wa Goli Bora la CAF 2022
Sakho alitajwa kushinda Tuzo hiyo usiku wa kuamkia leo katika shughuli maalum ya Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF iliyofanyika mjini Rabat nchini Morocco.
Mo Dewji ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumpongeza kiungo huyo aliyesajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu uliopita, huku akimshukuru kwa kuiheshimnisha Msimbazi na nchi ya Tanzania.
Mo Dewji ameandika: Wanasimba na Watanzania tunajivunia mafanikio yako mchezaji wetu Pape Sakho. Hongera kwa kushinda Tuzo ya Goli Bora la CAF 2022 na asante kwa kuleta heshima ya kipekee kwa Simba na Tanzania. Tuzo hii imezidi kuonyesha namna gani Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wenye viwango vikubwa! #nguvumoja
Sakho aliingia kwenye kinyang’anyirio cha kuwania Goli Bora la CAF 2022 kupitia bao alilofunga kwa ustadi mkubwa Mabingwa wa Ivory Coast ASEC Mimosas katika mchezo wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani humo msimu wa 2021-22.
Mchezo huo uliounguruma katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na kushuhudia Simba SC ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1, mabao mengine ya Mnyama yakifungwa na Shomari Kapombe na Peter Banda.
Mabao mengine ambayo yaliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Goli Bora la CAF 2022 yalifungwa na Gabadinho Mango wa Orlando Pirates ambapo bao lake alilifunga akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Malawi dhidi ya Morocco kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika AFCON 2022 zilizounguruma nchini Cameroon mwanzoni mwa mwaka huu 2022 na Zouhair El Mountaraji wa Wydad Athletic Club ambapo bao lake alilifunga kwenye mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly mwezi May.