Kiungo kutoka nchini Misri, Mohamed Elneny amsaini mkataba mpya wa mwaka mmoja wa kuendelea kuitumikia Arsenal.
Elneny mwenye umri wa miaka 30 ndiye mchezaji aliyekaa muda mrefu zaidi katika klabu hiyo, alijiunga na Washika Bunduki hao wa London kutoka FC Basel ya Uswizi, Januari 2016.
Kiungo huyo amecheza jumla ya michezo 155 katika mashindano yote, akifunga mabao sita na kutoa asisti 10 katika miaka saba aliyoitumikia Arsenal.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Mohamed Elneny alisema “Nina furaha sana, ninaipenda klabu hii pamoja na mashabiki wetu na nitajituma na kujitolea kwa nguvu zangu zote ili kuendelea kuwa bora zaidi.”
Kuhusu kuwa mchezaji aliyekaa muda mrefu zaidi, Kiungo huyo aliongeza: “Inanifanya nijivunie kuiwakilisha klabu hii tangu 2016. Roho na umoja tulionao katika kikosi chetu kwa sasa ni chanya na nina furaha kwamba nimeongeza mkataba.”
Nyongeza ya mkataba mpya wa Mohamed Elneny itamfanya kuendelea kusalia katika klabu hiyo hadi Juni 2024.