Mchezaji wa timu ya taifa ya Misri na klabu ya Liverpool, Mohamed Salah ametajwa kuwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2017 inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF).
Akitangazwa katika hafla ya utoaji tuzo kwa wanasoka zilizofanyika muda mfupi uliopita jijini Accra nchini Ghana, Mohamed Salah anabeba tuzo hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yake akiwafunika washindani wake katika kipengele hicho, Sadio Mane na Pierre-Emerick.
Salah mwenye umri wa miaka 25 ameibuka kidedea mwaka huu kutokana na kazi nzuri aliyoifanya mwaka jana akiifungia Liverpool magoli 17 katika michezo 21 baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea AS Roma.
Juhudi zake ziliisaidia Misri kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990, akipachika magoli katika mchezo kati ya nchi hiyo na Ghana pamoja na Burkina Faso.
Awali, wachezaji 30 walitajwa kuwania tuzo hiyo, lakini waliofanikiwa kuingia katika nafasi tatu za juu ni Salah, Aubameyang na Mane.