Klabu ya Soka ya AS Monaco imemsimmisha kazi kocha Thierry Henry kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake katika kuitafutia mafanikio uwanjani.
Hatua hiyo imetangazwa na AS Monaco kupitia taarifa kwa umma iliyowekwa kwenye tovuti yake, ikiwa ni siku tano tu tangu ipokee kipigo cha 5-1 kutoka kwa Klabu ya Strasbourg.
Katika mchezo huo ulioshuhudiwa Jumamosi ukiwaliza mashabiki wa timu hiyo, Henry alilazimika kuomba radhi kwa kutumia lugha isiyokubalika dhidi ya mlinzi wa Klabu ya Strasbourg, Kenny Lala.
Mabingwa hao wa Ufaransa wa mwaka 2017, wamejikuta wakipata rekodi mbovu ya kushinda michezo mitano kati ya 20 katika msimu huu, tangu Henry alipokabidhiwa mikoba Octoba mwaka jana. Wameshinda michezo miwili tu ya Ligi wakiwa na Henry.
Wakati Monaco wakieleza kuwa Henry ataendelea kusimama hadi watakapotangaza uamuzi kuhusu hatma yake ndani ya klabu hiyo, mikoba yake amepewa aliyekuwa msaidizi wake, Frank Passi.
Monaco ndiye muajiri wa kwanza aliyemkabidhi kikosi cha kwanza Henry anayekumbukwa kwa uwezo wake mkubwa akiwa na klabu ya Arsenal na timu ya Taifa ya Ufaransa.
Kazi yake ya awali kabla ya kukabidhiwa Monaco, ni kuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Ubelgiji iliyoshiriki Fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi.
Alijiunga na Monaco Oktoba 13 akichukua nafasi ya Leonardo Jardim, wengi wakiweka matarajio makubwa kwake, lakini leo maji yamemfika shingoni na anasubiri neno la mwisho kutoka kwa muajiri wake.