Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema suala la kiungo mshambuliaji Bernard Morrison ndani ya timu hiyo na kuwa Kwenye kikosi kitakachowavaa Singida United leo lipo mikononi mwa benchi la ufundi.
Morrison ameingia kwenye matatizo na Uongozi wa Young Africans na Benchi la Ufundi, kufuatia kuonyesha utovu wa nidhamu wakati wa mchezo wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) dhidi ya Simba SC Jumapili Uwanja wa Taifa.
Baada ya kufanyiwa ‘SUB’, Morrison ‘alimvimbia’ mwamuzi pale alipojaribu kumzuia asiondoke eneo la uwanja na hata kumsukuma na kuelekea katika vyumba vya kubadilishia nguo na kisha kuondoka moja kwa moja kwa usafiri wa Bodaboda.
Bumbuli amesema benchi la ufundi lina mamlaka ya kuamua kumrudisha kiungo huyo na kumtumia kwenye mchezo wa leo dhidi ya Singida United ambao utachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
“Suala la Morrison kuwa ndani ya kikosi ama kurejea kambini lipo mikononi mwa benchi la ufundi wao ndio watatuambia kama wanamhitaji au la kwani ndio kazi yao,” amesema.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa tangu Young Africans walipopoteza mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Simba SC kwa kuchapwa mabao 4-1 Julai 12, 2020, Morrison hajulikani alipo.
Kocha Luc Eymael amesema alipigwa simu na Morrison akiomba kurejea kuungana na wenzake lakini, akamtaka kwanza azungumze na viongozi na sio kumpigia simu yeye.