Katibu wa Geita Gold, Liberatus Pastory amesema ujio wa Kocha kutoka visiwani Zanzibar Hemed Suleiman ‘Morocco’ itasaidia kuirejesha timu yao kwenye anga za kimataifa kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Pastory amesema mipango ya msimu ujao ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza katika moja ya nafasi nne za juu, ambazo zitawasaidia kushiriki Michuano ya Kimataifa.

Morocco ametua kwenye kikosi hicho kuchukua nafasi ya Fredy Felix Minziro, ambaye amedumu kwenye kikosi hicho kwa misimu mitatu tangu ikiwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na sasa ikiitwa Ligi ya Championship.

“Tunaendelea na maandalizi ya msimu kwa kufanya usajili, maana tunaamini safari hii ligi itakuwa ngumu kuliko misimu yote tuliyoshiriki, hivyo lazima tuwe na maandalizi mazuri.

“Kambi tutakuwa hapa nchini, ila eneo inategemea kocha atapendekeza tukaweke wapi, hivyo uongozi utakuwa na kazi ya kuhakikisha tunakuwa pamoja na kocha katika kutimiza lengo la timu ambalo tumejiwekea,” amesema Pastory.

Morroco anakuwa kocha wa tatu kuifundisha timu hiyo tangu ipande Ligi Kuu, kwani kocha wa kwanza kuinoa alikuwa Etienne Ndayiragije, lakini baada ya kupata matokeo mabovu timu ikarejeshwa kwa Minziro.

Geita Gold ilipanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2021/22 pamoja na Mbeya Kwanza ambayo ilidumu msimu mmoja pekee kwenye ligi na sasa inashiriki Ligi ya Championship.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 15, 2023
Romelu Lukaku kuipa hasara Chelsea