Mchambuzi wa soka la Bongo Ally Mayayi Tembele amesema endapo Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes Darosa atampanga kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison kwenye mchezo dhidi ya Young Africans, itakua ni faida kubwa kwa klabu hiyo ya Msimbazi.
Simba SC watakuwa wenyeji wa Young Africans katika mchezo huo, ambao utaunguruma Jumamosi (Mei 08) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa akipewa jukumu la kupuliza filimbi.
Mayayi amesema Morrison ana umuhimu mkubwa kwenye kikosi cha Simba kwa msimu huu, na ameonesha usaidizi wa kuipa ushindi timu hiyo katika michezo kadhaa iliopita, hivyo kama atapewa nafasi ya kucheza taweza kufanya maajabu.
“Kwa tabia ya Morrison na mazingira ya mchezo wa mahasimu kama huo wa Mei 8 ni dhahiri ni mchezaji muhimu sana na ataisaidia timu kwa vitu tofauti. Akipewa nafasi atahitaji kuonyesha ubora, pia atahitaji kufanya jambo kubwa kwani tayari anaujua utamaduni wa soka letu.”
“Aidha, kiuchezaji, Morrison muda wote anataka kushambulia na huwa hatari zaidi kwa wapinzani, hivyo hiyo inaweza kuwa faida kwa Simba na kuwapa kazi ya ziada Young Africans katika mchezo huo.” Amesema Mayayi
Morrison ambaye alijiunga na Simba SC mwanzoni mwa msimu huu, baada ya sakata lake la Uongozi wa Young Africans kuchukua nafasi kubwa katika soka la Bongo, hajawahi kucheza mchezo wa ‘Kariakoo Dabi’ akiwa amevaa jezi za Msimbazi.
Mara ya mwisho kiungo huyo alicheza dhidi ya Simba SC akiwa kwenye kikosi cha Young Africans, na alifunga bao pekee la ushindi katika mchezo uliounguruma Machi 08, Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ulihudhuriwa na Hayati John Pombe Magufuli pamoja na aliyekua Rais wa CAF Ahmad Ahmad.
Simba SC inakwenda kucheza mchezo wa Jumamosi (Mei 08) ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufiksha alama 61, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 57 huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 54.