Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ghana Bernard Morrison hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC, kitakachoivaa Kagerea Sugar kesho jumatano kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.

Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomez Da Rossa amesema Morrison ambaye alitumika kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mwadui FC na kuchangia ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco, ataukosa mchezo huo kufuatia kuwa na kadi tatu za njano.

Moja ya kadi hizo alioneshwa kwenye mchezo dhidi ya Mwadui FC kufuatia kitendo cha kumsukuma Mwamuzi wa pembeni alipokua kwenye maandalizi ya kupiga mpira wa kona.

“Morrison ndiye atakosa mchezo wa kesho kwa sababu ya kuwa na kadi tatu za njano lakini wengine wote wako vizuri na hawa ambao hawapo kwenye mazoezi wamepumzika kwa sababu jumapili walicheza dakika 90” amesema Gomez.

Hata hivyo Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amefafanua kuwa moja ya mikakati yao ya kufikia malengo ya kushika usukani ni kupambana kila mechi kupata alama tatu na kwamba kutocheza kwa baadhi ya wachezaji si kwamba wana matatizo yoyote.

“Hao ambao hawajacheza si kwamba wana matatizo au siwaamini, kila mtu ana umuhimu wake kikosini na anatumika kulingana na mchezo husika ndio maana leo (jana) unaona mazoezini wapo hivyo anayeonesha uwezo namtumia” amesema Kocha Gomez.

Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 52, ikitanguliwa na Young Africans inayoongoza msimamo huo kwa tofauti ya alama mbili, huku Azam FC ikishika nafasi tatu kwa kufiksha alama 50.

UEFA: Tutaendelea kupinga European Super League
Muda mfupi baada ya kushinda Urais, Rais wa Chad auawa na waasi