Mshambuliaji kutoka nchini Zambia na Klabu ya Simba SC Moses Phiri amesema mafanikio yake msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, yatategemea sana ushirikiano mkubwa atakaoupata kutoka kwa Kiungo Clatous Chotta Chama.
Phiri ambaye hadi sasa ndio kinara wa upachikaji mabao kwenye kikosi cha Simba SC, amekuwa gumzo midomoni mwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo ya Msimbazi, kutokana na umahiri wake aliounyesha kwenye Michezo ya Ligi Kuu na ile ya Kimataifa.
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Zanaco FC ya nchini kwao Zambia, amesema itakua ngumu kwake kuendelea Kufunga na mwisho wa msimu kuwa Mfungaji Bora, kama atakosa ushirikiano kutoka kwa viungo wanaoongozwa na Chama aliyempachika jina la ‘Master’.
Amesema siku zote katika soka Mshambuliaji mwenye uchu wa kufunga, amekua akirahishiwa kazi na Viungo Washambuliaji, na kwa bahati nzuri Simba SC ina kiungo (Chama) mwenye sifa kubwa ya kutoa pasi za Mwisho, hivyo anamtegemea sana kuisaidia timu na kutimiza jukumu la kumaliza msimu akiwa kinara wa upachikaji mabao.
“Chama ndiye ninacheza naye pamoja pale mbele, yeye ni namba 10 na mimi 9, hivyo yeye ndiye atakayeamua kitakachotokea kwenye timu, na mwishoni mwa msimu kupitia mimi.”
“Nimekuwa nikifurahia kucheza na Chama kutokana na umahiri wake mkubwa wa kupiga pasi akifika katika goli la wapinzani na ninafurahia zaidi utulivu alionao.”
“Hivyo nishindwe mimi mwenyewe kutwaa ufungaji bora kama nikiendelea kucheza pamoja na Chama, ambaye kwangu ninamuona kama Namba 10 Bora katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.” amesema Phiri
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 hadi sasa ameshaifungua mabao manne Simba SC katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akifunga mabao matano kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.