Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri yupo mikononi mwa Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira kutokana na kupewa program maalumu itakayomrejesha kwenye ubora wake.
Desemba 21, mwaka jana, Phiri alipata maumivu ya mguu kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba walipotoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.
Baada ya hapo amekuwa nje akipambania hali yake na hata aliporejea uwanjani Februari 11, 2023 Uwanja wa General Lansana Conte dhidi ya Horoya alitumia dakika 29 alikwama kurejea kwenye hali yake ya kucheka na nyavu.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amesema Phiri ana program maalumu itakayomrejesha kwenye ubora, na msimu ujao atakuwa tayari kuipambania timu.
“Phiri alikuwa bado hajawa fiti baada ya kupata maumivu alipokuwa kwenye majukumu yake ya kazi ila kwa sasa ana program maalumu ambayo itamfanya arejee kwenye ubora.
“Ni matumaini yetu atakuwa fiti tayari kwa kuwapa furaha Wanasimba hivyo muhimu kuwa na subra kila kitu kitakuwa sawa.” amesema Ahmed Ally
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara Phiri amecheza michezo 18, kasepa na dakika 1537 akiwa amefunga mabao 10 na pasi tatu za mabao.