Mshambuliaji kutoka nchini Zambia na klabu ya Zanaco FC Moses Phiri amezima taarifa za kuwa kwenye mpango wa kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, huku akihusishwa kusaini kwa Mabingwa watetezi Simba SC.
Kiungo Mshambuliaji huyo ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Zanaco FC kilichocheza dhidi ya Young Africans siku ya Mwananchi mwaka 2021, amesema hafahamu kama atacheza Ligi ya Tanzania Bara msimu ujao ama kuendeleza kubaki nchini Zambia.
Amekiri ni kweli mkataba wake na Zanaco FC utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, lakini bado hajafahamu mustakabali wake kama ataendelea kubakia Zambia ama kuondoka na kwenda Tanzania, ambako anahusishwa nako kila kukicha.
“Mkataba wangu na Zanaco FC kweli unafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, bado sijasaini timu yoyote mpaka sasa ila naweza kwenda kucheza nje ya Zambia msimu ujao.”
“Mbali na kutarajia kutoka nje ya Zambia, pia ninaweza kubaki hapa kama nitapata ofa nzuri, mpira ndio ajira yangu kwa hiyo ofa yoyote ikijitokeza hata hapa na ikanitosha nitabaki.” Amesema Moses Phiri
Mbali na Simba SC klabu ya Young Africans nayo imewahi kutajwa kumuwania Kiungo Mshambuliaji huyo ambaye msimu huu alishindwa kuisaidia Zanaco FC kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.