Mshambuliaji kutoka Zambia na Klabu ya Simba SC Moses Phiri anamini ipo siku ataaminiwa na kupata nafasi ya kucheza na ndio hapo atakapomthibitishia Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’.
Mzambia huyo kwa sasa amepoteza nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza tangu alipata majeraha ya mfupa unaokaribia katika enka ya mguu kushoto, ambayo aliyapata katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, Desemba 2022.
Ugumu wa Phiri kuanza katika kikosi cha kwanza umeongezeka zaidi baada ya Simba SC kumsajili mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Baleke ambaye amekuwa na kasi ya juu ya kufunga kwa sasa.
Phiri amesema kuwa kikubwa ni kuweka malengo kwa yeye ili aingie katika kikosi cha kwanza timu hiyo, licha ya ugumu na ushindani uliokuwepo hivi sasa.
Phiri amesema kuwa bado anaendelea kupata maelekezo kutoka kwa kocha wake Robertinho ili aendane na mfumo, aina ya uchezaji anayoitumia ambayo anaona kwake ndio changamoto kubwa.
Ameongeza kuwa hakuna kitakachomshinda yeye kuingia na kucheza katika kikosi cha kwanza, kama aliwahi kuwepo katika michezo ya mzunguko wa kwanza wa ligi.
“Hakuna timu utakayokwenda na kukosa ushindani wa namba, kikubwa kinachotakiwa ni kupambana ili uingie hicho ndio ambacho nitakachokifanya kwa sasa.”
“Nafahamu ushindani wa namba umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika timu, hasa ongezeko la wachezaji katika dirisha dogo msimu huu,” amesema Phiri
Mshambuliaji huyo jana Ijumaa (Aprili 28) alipata nafasi ya kucheza dakika kadhaa katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad AC ya Morocco, huku akipata mkwaju wa Penati baada ya timu hizo kupata matokeo ya jumla ya 1-1.