Kocha wa Klabu Bingwa Barani Afrika Al Ahly SC Pitso Mosimane amewashukia baadhi ya Waandishi wa Habari wanaopinga mpango wake wa kumtumia Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbiji Jose Luis Miquissone.
Mosimane alimsajili Miquissone akitokea kwa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, wakati wa dirisha la usajili la msimu wa 2021/22.
Kocha huyo kutoka nchini Afrika Kusini aliwashukia Waandihi hao usiku wa kuamkia leo Jumanne (Novemba 23), baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Misri dhidi ya Ghazl El Mahalla, ambapo Al Ahly ilichomoza na ushindi wa mabao 2-3.
Mosimane aliwajibu kwa hasira Waandishi hao wa Habari baada ya kuhoji uwezo wa Luis Miquissone ambaye bado hajaonyesha makali yake tangu ajiunge na timu hiyo.
“Kwa hiyo unataka Luis asicheze, Kwa nini asicheze, mbona wachezaji wengine hujauliza, kwa nini Luis” “Ni nani aliyesababisha faulo ya ushindi, tumepata goli kutokana na kazi ya nani?”
“Luis ni mchezaji wa Al Ahly na atacheza hapa, atapata nafasi kama Hamdy, atapata nafasi kama wachezaji wengine, kila mmoja ni mchezaji wa Al Ahly, hapa atacheza”
“Nitamtoa Tau, nitamtoa Sherif na nitamtoa hata Afsha, hapa hakuna STAR, wachezaji wote ni sawa” alisema Mosimane