Watoto 11 waliokuwa wamehifadhiwa katika chumba maalum baada ya kuzaliwa wamefariki kwa ajali ya moto iliyotokea Hospitali ya Mkoa ya Mame Abdoul Aziz Sy Dabakh iliyopo kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu waSenegal, Dakar.
Rais wa nchi hiyo, Macky Sall ametoa taarifa ya tukio hilo akieleza kuhuzunishwa. Pia, Rais huyo ametuma salamu za rambirambi na pole kwa wazazi wa watoto hao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Mei 25, 2022 katika chumba cha idara ya watoto wachanga ya hospitali hiyo.
“Nimepokea kwa uchungu na mshtuko vifo vya watoto 11 waliozaliwa kufariki kwenye moto huko Tivaouane. Pole ziwafikie mama zao na familia zao, nina masikitiko makubwa,” amesema Rais Sall.
Awali, Waziri wa afya wa Senegal Abdoulaye Diouf Sarr akizungumza kupitia kituo cha televisheni, amesema uchunguzi wa awali unaonesha moto huo ulianza taratibu bila kugundulika haraka na kusababisha madhara hayo.
Amesema licha ya pole zilizotolewa na Rais wa nchi hiyo kwa wafiwa, pia amekatisha ziara yake na atarejea haraka kuungana na wananchi wake kwenye msiba huo.
“Vyombo vyetu vya usalama vinaendelea na uchunguzi lakini taarifa za awali ni kwamba huu moto ulianza taratibu bila kugundulika na kuleta madhara. Pia, nimewasiliana na Rais Sall yupo njiani kurudi kuungana na sisi,” amefafanua Waziri Sarr.
Kwa upande wake Meya wa jimbo la Tivaouane, Demba Diop Sy amesema kikosi cha polisi kwa kushirikiana wale wa zima moto bado wako hospitalini.
Amewataka wananchi kuwa watulivu wakiendelea kusubiri taarifa rasmi kutoka katika vyombo vya Serikali.