Bolivia imetoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa nchi tatu, utakaohusisha Brazil na Paraguay, kuzima moto unaoendelea kuteketeza kwa kasi kubwa msitu mkubwa dunani wa Amazon uliopo kati ya nchi hizo tatu.
Maafisa katika mkoa wa Santa Cruz, wanakadiria kwamba moto huo ulioenea maeneo mbali mbali ya mashariki mwa Bolivia, tayari umekwisha teketeza zaidi ya hekta 450,000.
Aidha, Jeshi la Bolivia linaendelea na juhudi za kuzima moto huo ambao umefikia sehemu ya daraja la Rio Negro, kati ya miji ya Puerto Suarez na Puerto Busch, mpakani mwa Brazil, Paraguay na Bolivia.
Hata hivyo, waziri wa ofisi ya Rais wa Bolivia, Huan Ramon Quintana, ametoa wito wa ushirikiano ili waweze kufanikiwa kuuzima moto huo huku moto huo ukitapakaa na kuendelea kuteketeza msitu huo wa Amazon.