Moto umezuka katika mlima Kilimanjaro karibu na eneo la Karanga Camp lililopo urefu wa meta 3,963 kutoka usawa wa bahari kupitia njia ya Mweka na jitihada ya kuuzima zinaendelea.
Kamishina wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi Tanzania (Tanapa), William Mwakilema amesema vikosi vinaelekea kuuzima moto huo.
Moto huo ulianza kuonekana jana Ijumaa Oktoba 21, 2022 usiku kutokea Moshi Mjini, ambapo kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi Kamishina wa Uhifadhi William Mwakilema amesema moto huo unadhibitiwa.
Taarifa zinaeleza moto huo unawaka ukanda wa Moorland, ambao mimea yake ikishika moto huwa ni mkali na tayari Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa) wametuma vikosi kwenda kuukabili.