Meneja wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekataa kuzungumzia kwa kina adhabu ya kadi nyekundu iliyomfika beki na nahodha wa kikosi chake John Terry, wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya West Brom uliounguruma jana jioni.

Mourinho, alikataa kuzungumzia suala hilo alipokutana na waandishi wa habari mara baada ya mtanange huo kumalizika ambapo Chelsea walifanikiwa kupata ushindi wa mabao matatu kwa mawili.

Terry, alikutwa na kadhia ya adhabu dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza, ambapo alifanya kosa la dhahir la kumshika na kumvuta kwa nyuma mshambuliaji wa West Brom, Salomon Rondon.

Alipoulizwa kama atakata rufaa kupinga adhabu hiyo, Mourinho alisema hatathubutu kufanya hivyo kwa sababu ni sawa na kazi bure, kutokana na kuamini wazi wahusika hawawezi kusikiliza maelezo yatakayotolewa kama utetezi.

Katika mchezo huo mshambuliaji mpya wa Chelsea, Pedro Rodrigues alifunga bao lake la kwanza baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na The Blues akitokea FC Barcelona mwishoni mwa juma lililopita.

Mabao mengine ya Chelsea yalifungwa na Diego Costa pamoja na Cesar Azpilicueta huku mabao ya kufutia machozi kwa wenyeji yakifungwa na James Morrison pamoja na James Morrison.

Ushindi huo unakua wa kwanza kwa The Blues tangu msimu huu ulipoanza majuma tatu yaliyopita, baada ya kushuhudia wakipoteza mchezo wao wa pili dhidi ya Man City na katika mchezo wa kwanza walilazimishwa sare mabao mawili kwa mawili dhidi ya Swansea City.

Ray C Afanya Documentary Ya Maisha Yake Ya Uteja
AC Milan Wadhamiria Kukilinda Kipaji Cha Balotelli