Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imeandaa mpango kabambe wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Bahari ya Hindi.
Khamis ameyasema hayo hii leo Mei 22, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Daudi Hassan aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kutenga fedha za mabadiliko ya tabianchi kusaidia wananchi wenye visima vya maji chumvi Zanzibar.
Amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inatekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa pande mbili za Muungano ambayo inahusika na uchimbaji wa visima.
“Kwa upande wa Zanzibar, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBBAR) umechimba visima sita katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) umechimba visima viwili katika Shehia ya Maziwa Ng’ombe na Shehia ya Kiuyu Mbuyuni katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini, Pemba,” alisema.
Aidha, amesema Serikali imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa kuta za bahari Mikindani (Mtwara) na Sipwese (Pemba) ili kupunguza kasi maji chumvi kutoka baharini kuingia kwenye makazi ya wananchi.