Kuanzishwa kwa program za kudhibiti kuenea kwa virusi aina ya Rabies vinavyosababisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ni mfano bora wa utekelezaji wa mradi wa Afya na utokomezaji wa magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ambapo kwa Tanzania watu 15,339 wakiripotiwa kuumwa na Mbwa kati ya Januari hadi Agosti 2022.
Hayo, yamebainishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO), katika siku ya kichaa cha Mbwa Duniani (Septemba 28,2022), na takwimu hizo za Tanzania zikitolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichalwe ambazo hata hivyo zimepungua kutoka matukio 39,787 yaliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2021.
Shirika hilo linasema, kwa kuwa tayari dunia ina chanjo, dawa, mbinu na teknolojia za kuvunja mzunguko wa ugonjwa huo ambao ni moja ya magonjwa ya zamani, waathirika wengi wa ugonjwa huo ambao mbwa ndio chanzo chake kikuu ni watoto katika jamii maskini kwenye mabara ya Afrika na Asia.
Kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya Rabies, ingawa una chanjo bado unapatikana katika nchi na maeneo zaidiya 150 duniani na licha ya kuwa na kinga bado unasababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu kila mwaka hususan Asia na Afrika na kusababisha hasara ya dola bilioni 8.6 za matibabu, na nguvu kazi inayopotea.
Asilimia 40 ya watu wanaong’atwa na wanyama wanaosambaza ugonjwa huo wakiwemo mbwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 huku Barani Amerika popo nao wakitajwa kuwa chanzo kikuu cha maambukizi ya ugonjwa huo kutokana na maambukizi ya mbwa kudhibitiwa kwenye eneo hili.
Maambukizi kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu yanaweza kutokea pia iwapo mnyama mwenye virusi hivyo atagusana na kidonda kibichi cha binadamu, huku WHO ikisema kipindi cha virusi kushamiri mwilini na dalili huanza kuonekana kati ya miezi 2 hadi 3, wiki moja hadi mwaka mmoja kulingana na vigezo mbalimbali ikiwemo ni eneo gani virusi vimeingilia mwilini na kiwango chake.
Nchini Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hezron Nonga anasema kwa wastani watu 3,387 hung’atwa na mbwa kila mwaka, hivyo kuwa kwenye hatari ya kuambukizwa kichaa cha mbwa kinachoenezwa pia na mbwa mwitu, paka, fisi na popo.
Amesema, “Mbwa na paka wanaozurura ovyo, anasema ndio waenezaji wakubwa wa kichaa cha mbwa na binadamu anaweza kuambukizwa kwa kugusa mate ya mnyama aliyeathirika, kupitia jeraha, mchubuko, jicho, pua au mdomo, na kwamba kanuni ya uchanjaji wa mifugo ya mwaka 2020 inamlazimu kila mfuga mbwa au paka kumchanja ili kuzuia kichaa cha mbwa na kinyume cha hapo adhabu yake ni faini ya kati ya Shilingi 500,000 hadi milioni 10, au kwenda jela mwaka mmoja.”