Wadadisi wa masuala la soka nchini Hispania wamebaini wazi kuwa, beki wa kutumainiwa wa mabingwa wa La Liga “FC Barcelona” Gerard Pique alifanya makusudi kujitafutia kadi ya njano, wakati wa mchezo dhidi ya Sevilla siku ya jumapili.
Taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zimeainisha kuwa, Pique alifanya hivyo kwa kuhisi huenda angeukosa mchezo dhidi ya Real Madrid “El Clasico” ambao ni muhimu kwa kila mchezaji wa pande hizo mbili kuucheza, ili kuweka historia.
Beki huyo alionyeshwa kadi ya njano, baada ya kuupiga mpira kwa makusudi, ili hali akifahamu kanuni hazimruhusu mchezaji kufanya hivyo, baada ya mwamuzi kupuliza kipyenga.
Kwa hatua ya kuonyeshwa kadi ya njano, kulimfanya beki huyo mwenye umri wa miaka 32, kufikisha idadi ya kadi tano, ambazo zinamnyima nafasi ya kucheza mchezo ujao dhidi ya Eibar, na baada ya hapo atakua huru kuanza kuhesabiwa upya idadi ya kadi kama hizo.
FC Barcelona watacheza dhidi ya Eibar baada ya mapumziko ya michezo ya kimataifa, na siku tano baadae watashuka dimbani kuwakabili Real Madrid kwenye dimba la Camp Nou.