Serikali imezindua mpango mkuu wa maendeleo wa sekta ya fedha wa miaka 10 (2020-2030).
Mpango huo una lengo la kuongeza wigo na fursa za upatikanaji huduma za kifedha kwa wananchi, zikiwemo za bima, mikopo, akiba na uwekezaji.
Aidha mpango huo unalenga kuongeza mchango wa huduma za kifedha na bima kwenye Pato la Taifa (GDP), ambao kwa miaka mitano iliyopita umeendelea kuwa na wastani wa asilimia 3.5 kiasi ambacho bado ni kidogo.
Akizindua mpango huo kwa niaba ya katibu mkuu Hazina Doto James, Naibu katibu mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango Mary Maganga, amesema kuwa kwa sasa ni asilimia 8.6 tu ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za kibenki ikilinganishwa na asilimia 32.1 wanaoishi mjini .
Alisema mpango huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi na viwanda.
Aidha, Maganga ametoa rai kwa sekta hiyo kuendelea kuongeza ubunifu katika utoaji huduma za fedha ili kuboresha huduma kwa wateja, kuongeza vipato, kulipa kodi na kuchangia maendeleo ya Taifa.