Marilou Danley ambaye ni mpenzi wa Stephen Paddock aliyeua watu 58 na kujeruhi mamia kwa kuwashambulia kwa risasi katika tamasha la muziki la Las Vegas, amelipa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) taarifa kuhusu mtu huyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na FBI na Mwanasheria wa Danley ambaye alirejea kutoka jijini Manila nchini Ufilipino siku chache baada ya kutokea shambulio hilo, amesema kuwa hakufahamu lolote kuhusu mpango wa Paddock.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa anampenda na kwamba alikuwa mtu mkimya na mwema ambaye alikuwa anatumaini wangekuja kuishi maisha mazuri ya ndoa katika siku za usoni.

Danley ameeleza kuwa awali Paddock alimpa tiketi ya ndege akimtaka akaitembelee familia yake nchini Ufilipino. Akiwa nchini Ufilipino, alimtumia tena kiasi cha $100,000 ambazo alimtaka anunue nyumba jijini Manila.

“Nilishukuru sana kwa msaada wake, lakini kwakweli nilipata wasiwasi kuwa labda ilikuwa njia ya kutaka kuachana na mimi,” alisema Danley.

“Haikuwahi kutokea kwa namna yoyote kufikiria kuwa alikuwa anapanga kufanya tukio baya dhidi ya mtu yeyote,” aliongeza.

Msemaji wa FBI, Aaron Rouse amesema kuwa hadi sasa hawajapata sababu yoyote ya kuliunganisha tukio hilo na ugaidi lakini wanaendelea na uchunguzi bila kufunga milango ya taarifa za aina yoyote.

Hili ni tukio baya zaidi la mtu mmoja kuifyatulia risasi halaiki lililofanywa nchini Marekani.

Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye alitembea eneo hilo jana alisema, “Marekani ni taifa ambalo hivi sasa liko kwenye maombolezo.”

DC Hapi atishia kufuta leseni za wamiliki wa hoteli
Video: Gongo yaua watu 19 Dar, Siku 30 moto CCM, Ukawa