Aliyekuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa tiketi ya chama cha upinzani, Martin Fayulu amefungua kesi katika Mahakama ya Kikatiba akipinga matokeo ya uchaguzi wa nchi hiyo.
Tume ya Huru ya Uchaguzi ya Taifa (CENI), ilimtangaza mgombea mwingine wa upinzani Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Desemba 30 mwaka jana.
Kwa mujibu wa takwimu za CENI, Tshisekedi alipata kura milioni 7 huku Fayulu akipata kura milioni 6.4 na mgombea wa chama tawala mmanuel Shadary akiambulia kura Milioni 4.4.
Feli Ekombe ambaye ni mwanasheria wa Fayulu amesema kuwa katika kesi hiyo, mteja wake anataka Mahakama ifute matokeo yaliyotangazwa na CENI yanayombua Tshisekedi kama Rais mteule wa taifa hilo la Afrika ya Kati.
Marekani, Ufaransa na Uingereza vimetaka kutoa ufafanuzi wa kina wa namna matokeo hayo yalivyopatikana.
Wiki iliyopita, Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo, kupitia kwa Baraza la Maaskofu lilieleza kuwa matokeo yaliyotangazwa hayaendani na kile ambacho timu yake ya waangalizi 40,000 ilikipata.
Tshisekedi anatarajiwa kuapishwa Januari 25 mwaka huu kuwa Rais wa kwanza aliyekabidhiwa madaraka kwa kushinda uchaguzi.