Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ametoa rai kwa wadau wote wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote nchini wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Ameyasema hayo wakati akizindua mradi wa Jifunze Uelewe wenye lengo la kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa awali hadi darasa la nne katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Mtwara na Ruvuma wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Uzinduzi wa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) umefanyika katika shule ya Albert Luthuli mkoani Morogoro ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha utoaji elimu nchini kwa kuhakikisha mazingira salama na jumuishi katika kusoma kwa watoto.
Amesema mradi huo utatoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini 25,578 katika shule 2,825 na kwamba utanufaisha jumla ya wanafunzi 1,259,227 kutoka katika mikoa hiyo.
“Niwaombe wadau wote wa elimu, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni binafsi na vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha ushiriki wa pamoja ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum,” Amesema Prof. Ndalichako.
Awali, akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la USAID, Kate Somvongsiri amesema mradi wa Jifunze Uelewe utahakikisha wanafunzi wa awali hadi darasa la nne wanapata nyenzo za kujifunzia katika muundo wa machapisho na dijitali ili kuimarisha mtaala na kutoa fursa kwa mazoezi ya kujitegemea.
Naye Germana Mung’aho ambaye ni Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huyo, ameishukuru Serikali na Shirika la USAID kwa kuona umuhimu wa kuinua elimu mkoani humo na kuahidi kushirikiana bega kwa bega katika kutekeleza mradi huu ili kufikia malengo yaliyowekwa.