Wafanyakazi 16 wa bandari iliyopata mripuko katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut uliopo katika pwani ya bahari ya Mediterania wamekamatwa, zikiwa zimepita siku mbili pekee tangu kutokea kwa mripuko huo.
Kwa mujibu wa mwanasheria mkuu wa jeshi la nchi hiyo Faki Akiki, uchunguzi unafanyika unahusisha maafisa wa bandari pamoja na maafisa wa forodha.
Imeelezwa kuwa Serikali ya Lebanon, ambayo inakabiliwa na mkandamizo mkubwa kutoka kwa umma wa nchi hiyo, wameahidi kutoa maelezo ya haraka kuhusiana na chanzo cha mripuko huo.
Wengi wa wananchi wa nchi hiyo wanataka ufanyike uchunguzi wa kimataifa. Wafanyakazi wa uokozi wanajaribu kuwatafuta watu 100 ambao hawajulikani waliko. Idadi ya watu waliofariki kwa mujibu wa wizara ya afya imepanda na kufikia watu 149.