Uongozi wa Azam FC, umesema kwa sasa uko katika mchakato wa kukamilisha usajili wa beki wa kushoto kutoka nchini Cameroon kuja kuchukua nafasi ya Bruce Kangwa aliyepewa mkono wa kwa kheri.
Azam FC tayari wametangaza nyota wawili ambao wamekamilisha usajili wao akiwemo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kiungo Djibril Sillah anayetarajiwa kutua nchini leo Ijumaa (Juni 30) kwa ajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Azam FC juzi iliweka wazi kiungo huyo kutoka Raja Casablanca anakuja kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho ambacho kimekosa ubingwa msimu wa 2022/23.
Afisa habari wa klabu hiyo, Hashim Ibwe amesema baada ya kukamilisha usajili wa kiungo huyo sasa wako kwenye hatua za mwisho kumalizana na beki wa kushoto kutoka timu ya taifa ya Cameroon ambayo alicheza CHAN.
Amesema wanatengemea kusajili wachezaji wawili wa kigeni na wamejipanga vizuri kufanya usajili mzuri na wenye malengo na kuhakikisha wanakuwa tishio kwenye kuwania mataji yote msimu ujao.
“Tumefanya usajili mzuri na mashabiki wa Azam FC msimu huu watajipiga kifua kwani tumejiimarisha kwa michuano yote iliyopo mbele yetu ikiwemo Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ pamoja na kombe la Shirikisho Barani Afrika,” amesema Ibwe.