Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamemtangaza Andrew Mtine kutoka nchini Zambia kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa klabu hiyo akichukua nafasi ya Senzo Mbatha.
Mtine amrtengazwa rasmi leo Jumanne (Septemba 27) huku akipewa mkataba wa miaka miwili, ambao unatarajiwa kutoa matokeo chanya ya kuisogeza mbele Young Africans kimaendeleo.
Baada ya kutambulishwa Jijini Dar es Salaam, Mtine ameahidi kuifanya Young Africans kuwa klabu kubwa zaidi Barani Afrika.
“Nina uzoefu mkubwa na kazi nimefanikiwa kupita sehemu mbalimbali ikiwemo kuwa kwenye uongozi wa Shirikisho la Zambia na pia nimewahi kufanya kwenye klabu ya Zesco ya Zambia pamoja TP Mazembe ya nchini Congo hivyo najua nilichokuja kukifanya” anaendelea na kusema
“Nimekuja kutimiza malengo ya Young Africans, kiu yangu ni kuona ikifika mbali na kujulikana kimataifa jambo ambalo nalitamani pia,”
“Young Africans ni timu kubwa sana, nimekuwa naifuatilia kwa muda sasa. Nimejifunza kuwa ni timu kubwa, na tunaweza kuifanya kuwa kubwa zaidi, siyo tu ukanda wa Afrika Mashariki bali kuwa klabu kubwa zaidi Afrika,” amesema Mtine
Miongoni mwa majukumu ya Mtendaji Mkuu katika timu ni: Kusimamia maamuzi ya kampuni ili yafanyike kama ilivyoamuliwa katika vikao vya ndani vya bodi au mkutano mkuu wa kampuni amabpo anakuwa kiunganishi kati ya pande zote mbili hususani kufikia maendeleo ndani ya Yanga katika malengo yake ya muda mfupi na muda mrefu.
Kazi ya pili la CEO ni kusimamia operesheni zote za kampuni na mali zake. Operesheni kubwa ya Young Africans kwa sasa ni kuhakikisha wanafanya vyema katika Michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pia CEO ana jukumu la kuhakikisha kampuni inakuwa na mawasiliano mazuri na wawekezaji wake. Hivyo Mtine ana jukumu la kuhakikisha menejimenti ya Young Africans inakuwa katika mahusiano mazuri ya kiutendaji.