Tanzania imepatiwa msaada wa shilingi bilioni 210 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta za afya, maji, utalii, mazingira, utawala bora, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuboresha mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kufuatilia matukio ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Msaada huo, umetangazwa kutolewa jijini Berlin mara baada ya kukamilika kwa majadiliano kati ya ujumbe wa Tanzania chini ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba na Ujumbe wa Ujerumani ulikuwa chini ya Naibu Waziri anayesimamia uhusiano wa kiuchumi na Maendeleo wa nchi, Dkt. Barbel Kofler.
Akiongea mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Nchemba amesema, “Serikali ya Tanzania inafuraha kupokea msaada wa Euro milioni 87 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 210, utakaosaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha Maisha ya watu.”
Ameongeza kuwa, sehemu ya msaada huo pia itaelekezwa kwenye jamii ikiwemo usawa wa kijinsia, kuimarisha haki za wanawake na Watoto kwa kuzuia kila aina ya vitendo vya ukatili dhidi yao ili kuharakisha maendeleo ya nchi.