Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, limesema limeanza oparesheni maalum ya kuwasaka wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kama vile wizi na itendo vilivyo kinyume na muenendo mwema wa maadili ya Kitanzania.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisin Benjamin Kuzaga alisema hayo Alhamisi Novemba 2, 2023 wakati akizungumza na Wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Mbeya.
Amesema, “Mkoa wa Mbeya kuna tatizo la wanafunzi wa vyuo vikuu kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani wanafunzi wa mwaka wa kwanza na kusababisha kupoteza mwelekeo, hili halitavumilika na msako umeanza mjiepushe la sivyo wote wenye tabia kama hii watajutia.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Jamii na kaimu Mkuu wa Chuo, John Jorojick ameonya wanafunzi waliopata fursa ya masomo kwa mwaka wa kwanza, kuepuka vitendo viovu ikiwemo kujiuza na uhalifu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia yupo katika ziara ya kutembelea na kutoa elimu ya usalama kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na vyuo, kwa lengo la kuzuia uhalifu hasa unaojitokeza maeneo ya masomo.