Mbunge wa Iringa Mjini – CCM, Jesca Msamtavangu amezungumzia suala la kikokotoo Bungeni jijini Dodoma na kusema tatizo si elimu bali malalamiko juu ya asilimia ya kikotoo inayotolewa kwa mafao ya mkupuo.
Akiuliza swali la nyongeza leo Jumanne Mei 9, 2023, Mbunge huyo amesema, “lini Serikali itafanya ujumuishi, wapo waliokuwa NSSF wakaenda PSSSF wakalipwa kidogo lakini wanatakiwa kwenda tena kufuatilia NSSF, mmejipangaje kuwasaidia ili walipwe kwa pamoja.”
Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akijibu swali hilo, alisema awali wastaafu waliokuwa wakilipwa kwa kikitoo cha asilimia 25 walikuwa wanapata mafao ya Shilingi 44 milioni na pensheni ya Shilingi 800,000 kila mwezi.
Amesema, mabadiliko katika kanuni hiyo, ambayo yanatoa mafao ya mkupuo kwa asilimia 33, mstaafu aliyekuwa akipata Shilingi 44 milioni ambapo kwa sasa anapata Shilingi 58 milioni na Pensheni ya zaidi ya Shilingi 700, 000.