Mwanamuziki wa Uganda, Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine ameshinda ubunge wa jimbo la Kyadondo Mashariki, kupitia uchaguzi mdogo.
Bobi Wine ambaye alikuwa mgombea binafsi asiye na chama katika uchaguzi huo, alitangazwa kwa kupata ushindi mkubwa wa kura 25,659 kati ya kura 33,310 zilizopigwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Uganda la New Vision, baada ya kutangazwa kuwa mbunge mpya wa jimbo hilo alisema kuwa kazi yake ya kwanza ni kuhakikisha anawaunganisha viongozi wa jimbo hilo kama ambavyo muziki huwaunganisha watu.
“Kitu cha kwanza nachotaka kukifanya ni kuwaunganisha viongozi wa Kyadondo Mashariki. Nataka siasa iwalete watu pamoja kama muziki ulivyofanya,” alisema Wine.
Uchaguzi huo mdogo ulifanyika baada ya mahakama nchini humo kuamua kuwa uchaguzi ulifanyika mwaka jana jimboni hapo ulivunja kanuni.
Bobi Wine alikutana na changamoto kadhaa wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na kuwekwa selo kwa kosa la kufanya mkutano karibu na eneo ambalo Rais Yoweri Museveni alikuwa akifanya mkutano kumnadi mgombea wa chama chake, kinyume na utaratibu uliokuwa umetolewa na jeshi la polisi.