Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amesema kuwa Bohari ya dawa inatarajia kuanza ujenzi wa kituo cha mauzo na usambazaji dawa mkoani Simiyu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa mkoa wa Simiyu na mikoa jirani.
Ameyasema hayo Agosti 19, 2019 mkoani humo katika ufunguzi wa mkutano wa tathmini ya utendaji kazi wa menejimenti na mameneja wa kanda wa bohari ya dawa nchini, lengo likiwa ni kujenga ushirikiano na kufanya kazi kwa timu.
Amesema kuwa wameamua kufanyia mkutano wa tathmini mkoani Simiyu ili kuweza kujionea eneo la ujenzi wa kituo cha mauzo ya dawa ikiwa ni moja ya kuongeza wigo mpana wa utoaji huduma.
“Tutakuwa na mkutano wa siku tatu hapa Simiyu kwa ajili kufanya tathmini ya utendaji kazi ulivyokuwa kwa mwaka mzima, tutawafanyia tathmini wakurugenzi wote na wenyewe watamfanyia Mkurugenzi Mkuu, lakini pia tutatumia fursa hii kutembelea mahali tulipoamua kujenga bohari kwa kuwa tunatarajia kujenga bohari hapa Simiyu,”amesema Bwanakunu.
Akifungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesema kuwa maboresho ya usambazaji wa dawa yaliyofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) yameongeza upatikanaji wa dawa mkoani Simiyu ambapo kwasasa upatikananji wa dawa ni zaidi ya asilimi 88.
Aidha, Sagini ametoa wito kwa Taasisi zote za Umma zinazohitaji maeneo kwa ajili ya kujenga Ofisi zao kufika mkoani Simiyu, ambapo amewahakikishia upatikanaji wa maeneo lengo likiwa ni kuendelea kusogeza huduma mbalimbali karibu na wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Bohari ya Dawa (MSD), Victoria Elangwa amesema kuwa uwepo wa kituo cha kusambaza dawa Simiyu kutapunguza umbali kwa Mkoa wa Simiyu na mikoa ya Mara na Shinyanga kupata huduma za Bohari ambazo kwa sasa zinapatikana Mwanza.
Ameongeza kuwa ujenzi wa Kituo hicho unatarajia kuanza mara moja kwa kuwa tayari wataalam wameshaanza kushughulikia masuala ya ukamilifu wa mazingira na baada kukamilisha kazi hiyo atatafutwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi.