Msemaji Mkuu wa Serikali amepongeza juhudi za zinazofanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa juhudi kubwa za uhifadhi zilizosaidia kuongeza idadi ya Watalii wanaotembelea hifadhi hiyo mwaka huu.
Amesema hayo leo machi 28,2022 mara baada ya kutembelea hifadhi ya eneo la Ngorongoro Mkoani Arusha ili kujionea hali halisi ya uhifadhi na mwitikio wa Watalii wanaotembelea hifadhi hiyo baada ya Serikali kuchukua hatua madhubuti za uhifadhi.
Msigwa amesema juhudi za kuilinda ikolojia ya Serengeti zimesaidia kuimarisha vivutio vilivyopo katika ikolojia hiyo likiwemo eneo la Ngorongoro, pori tengevu la Loliondo, pori la akiba la Maswa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo wananchi kutoa ushirikiano katika juhudi hizo ili kulinda maeneo ya hifadhi ambayo yanatoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kupitia mapato ya utalii.
Juhudi za Serikali kulinda hifadhi za Taifa na kutekeleza matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kukabiliana na janga la Uviko-19 zimesaidia kuongeza idadi ya Watalii msimu huu hadi kufikia 1,700,000 ikilinganishwa na Watalii 620,000 wa msimu uliopita.