Mbunge wa Iringa mjini, Jesca Msambatavangu amewaasa Wananchi kuacha ulalamishi na badala yake wayalinda na kuyatunza mazingira yanayowazunguka akisema faida zake ni kwa ajili ya uhai wao si Serikali peke yake, kama baadhi ya watu wanavyofikiri.
Msambatavangu ameyasema hayo mjini Iringa hivi karibuni katika mahojiano maalum na Dar24 Media na kudai kuwa Serikali na Wadau wa Mazingira wanapopaza sauti juu ya utunzaji na uhifadhi wa Mazingira hawafanyi hivyo kwa ajili yao bali kwa ajili ya jamii.
“Watu wanalalamika kuhusu mgao wa umeme, uhaba wa mvua wengine kukosa mazao kwa uhakika, sababu ni uharibifu wa Mazingira maana mabwawa yanayochangia uzalisha wa umeme yamekauka au kupungua maji tujirekebishe,” amebainisha Msambatavangu.
Aidha, Mbunge huyo amebainisha kuwa vyanzo vingi vya maji na ukosefu wa mvua za uhakika umekuwa ukisababishwa na baadhi ya watu wasio waaminifu kuharibu mazingira na ukataji hovyo wa miti, kitu ambacho hakifai na kinapaswa kukemewa.
Serikali, kupitia mamlaka mbalimbali na wadau wa Mazingira wamekuwa wakipaza sauti juu ya suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira, huku vyombo vya Habari ikiwemo Dar24 vikiendelea kuuhabarisha, kuuelimisha na kuutaka umma kupambana ili kulinda mazingira.