Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza katika maeneo yao vinginevyo watanyang’anywa.
Ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa kikao cha Rais Magufuli na wafanyabiashara kilichokuwa na lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali, ambapo amewataka wafanyabiashara hao kuwekeza katika maeneo yao.
Amesema kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa katika sekta ya ardhi, hivyo wanapaswa kufuata sheria na taratibu za nchi kwani vinginevyo ardhi hizo zitafutwa.
”Niwatake wafanyabiashara wote na wawekezaji mfike serikalini ili muweze kumilikishwa ardhi na si vinginevyo tutaifisha tu hiyo ardhi, njooni serikalini ili mfuate utaratibu uliowekwa ili kuweza kuondoa migongano,”amesema waziri Lukuvi
Aidha, katika mkutano huo, waziri Lukuvi amefuta heka elfu moja za mfanyabiashara na muwekezaji mmoja anayejulikana kwa jina na Kalua baada ya kuonyesha ametumia udanganyifu katika umiliki wa eneo hilo.
Hata hivyo, Lukuvi amezitaka taasisi mbali mbali zinazohusika na ardhi kuhudhuria jijini Dodoma kwaajili ya kutatua kero mbalimbali zinazoikumba wizara ya ardhi katika nyanja tofauti tofauti.