Kiungo Mshambuliaji kutoka Tanzania Simon Msuva ni kama ameyatega Manguli wa Soka la Bongo Simba SC, Young Africans na Azam FC, katika kipindi hiki cha usajili kuelekea msimu ujao 2023/24, kwa kujitangaza yupo huru.
Msuva ambaye aliifungia Taifa Stars bao la ushindi katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Niger mwishoni mwa juma lililopita (Jumapili- Juni 18), ametoa kauli hiyo baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Al-Qadsiah FC ya Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia.
Mtihani wa kwanza kwa Manguli ya Soka la Bongo kumsajili Mshambuliaji huyo upo katika maslahi binafsi ya Msuva ambaye alikuwa akilipwa mshahara mkubwa Al-Qadsiah FC, huku akiwa na ofa mkononi ya Al Duhail ambayo anaichezea Mkenya, Michael Olunga huko nchini Qatar.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Qatar, inaelezwa wapo tayari kumfanya mshambuliaji huyo ambaye alikuwa akiichezea kuwa mmoja wa wachezaji ghali kwenye kikosi hicho.
Kwa mujibu wa viwango vya malipo ya mishahara ya wachezaji wa Al Duhail miongoni mwa wachezaji ambao wanavuta mkwanja mrefu ni pamoja na Edmilson Junior ambaye aliwahi kutamba Ubelgiji akiwa na Standard Liege, anakusanya Pound 81, 000 (Zaidi ya Sh. 2479 milion) kwa mwezi.
Kiwango ambacho Al Duhail inataka kumpa Msuva kwa mwezi ni mara tano ya kile ambacho alikuwa akilipwa na Al-Qadsiah FC ambao nao wanapambana kuhakikisha mshambuliaji huyo anasalia kwenye klabu yao.
Msimu licha ya ugeni wake huko Saudi Arabia Msuva aliibuka kuwa mfungaji bora wa Al-Qadsiah FC na amethibitisha uwepo wa ofa kwenye mataifa ya China, Saudi Arabia na Qatar.
“Zipo timu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kunisajili, tusubiri tuone nini ambacho kitatokea, mkataba wangu ulishamalizika.”