Mfungaji wa wa bao pekee la Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ kwenye mchezo wa Kundi F wa kuwania Fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, Simon Msuva amesema amefurahi kutimiza ahadi yake ya kuitungua Uganda nchini Misri, lakini akisisitiza hata watakaporudiana nao watawapiga tena.

Msuva aliyefunga bao hilo kwenye Uwanja wa Suez Canal, Ismailia na kufikisha jumla ya mabao 20 kupitia michezo 77 aliyocheza akiwa na Taifa Stars, kabla ya mchezo huo nyota huyo anayekipiga Saudi Arabia alitamani sana kuifunga Uganda na kuahidi kupambana kutimiza lengo ili kuivusha Stars.

Ushindi wa Ijumaa (Machi 24) ulikuwa wa kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi F, kwani ilianza na sare ya 1-1 na Niger ugenini kabla ya kucharazwa mabao 2-0 nyumbani na kinara, Algeria na kesho Jumanne (Machi 28) itarudiana na The Cranes ili kufufua matumaini ya kwenda AFCON 2023 kwa mara ya tatu. 1980 Kwa mara ya kwanza Taifa Stars ilifuzu kucheza AFCON na mara ya pili ilikuwa 2019.

“Nimefurahi kuwa sehemu ya matokeo tuliyoyahitaji, sote tunafahamu ubora wa Uganda, hivyo sherehe ya matokeo ya mchezo huu imemalizika na sasa tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wa nyumbani, nikiamini tukikomaa tena tunawapiga ‘The Cranes’” amesema Msuva nyota huyo wa zamani wa Moro United, Young African, Difaa el Jadida na Wydad Casablanca zote za Morocco.

Msuva amesema anaamini Stars itapata ushindi nyumbani na kukusanya alama za kwenda Ivory Coast na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu hiyo ambayo ilishiriki Fainali za AFCON 1980 zilizofanyika Nigeria na Misri mwaka 2019.

“Sisi tupo kwa ajili ya nchi, tunahitaji sapoti ya mashabiki kwa sababu wao wana mchango mkubwa, muda mwingine mashabiki wanaweza kuwavuruga wapinzani kwa kuwatoa nje ya mchezo na kutufanya tuwe na kazi nyepesi,” amesema

Ni timu mbili tu zinafuzu kwa kila kundi na ushindi wa Ijumaa (Machi 24) umeifanya Stars ichupe hadi nafasi ya pili ikifikisha alama nne ikiishusha Niger yenye alama mbili iliyofumuliwa na vinara wa kundi hilo, Algeria yenye pointi tisa kwa sasa, huku Uganda ikiburuza mkia ikiwa na alama moja tu na kila timu ikicheza michezo mitatu kwa sasa.

Wezi wajisalimisha Polisi, walia kama watoto
Agizo la Rais huwa halipingwi: Waziri Mkuu