Mtambo unaotumia hewa tiba yenye mgandamizo ya Oksijeni (Hyperbaric Medicine Treatment), ambao unatibu magonjwa zaidi ya 10 umezinduliwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ya pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia mtambao huo.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Mtambo huo hii leo Desemba 13, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema kupitia matibabu haya mgonjwa huingizwa kwenye kifaa maalumu na kupatiwa tiba kupitia hewa tiba ya oksijeni iliyogandamizwa kwa asilimia 100.
Wagonjwa watakaonufaika ni wale wenye vidonda sugu ambavyo matibabu mengine yameshindikana kama wagonjwa wa sukari (diabetic foot), walioathirika na moshi baada ya kuungua na moto (carbon monoxide poisoning) na waliopata changamoto za upungufu wa oksijeni mwilini kama waliozama kwenye maji baharini n.k (decompression syndrome).
Amesema, wagonjwa wengine ni pamoja na walioungua na moto (acute thermal injury), wenye upungufu mkubwa wa damu ambao kwa njia moja au nyingine hawawezi kuongezewa damu, waliopata ajali na kupata majeraha mwilini yasiyopona na wagonjwa wenye maambukizi kwenye mifupa isiyopona.
Aidha, Prof. Janabi amesema, Wagonjwa wengine waliopata mionzi na kusababisha sehemu zilizopata tiba mionzi kuathitika ikiwemo wenye saratani za koo, njia ya chakula na wale wenye tezi dume, waliofanyiwa upasuaji na kuwekewa au kupandikiziwa sehemu ya miili yao, wenye changamoto ya kusikia ambao vipimo vimeshindwa kuonyesha tatizo, wenye tatizo la usaha kwenye ubongo, wenye changamoto ya Oksijeni kwenye mishipa ya damu na watoto wenye usonji.