Mwanasayansi wa Tanzania, Dkt. Joyce Singano amekuwa Mwafrika wa kwanza kupata Medali ya Brady inayotolewa kwa watafiti wa miamba.
Tuzo hii ni kubwa zaidi miongoni mwa tuzo zinazotolewa kwa watafiti wa ukadiriaji wa miamba wanaotumia visukuku viumbe ambao wanapatikana ardhini. (wanasayansi wa Micropaleontolojia).
Micropaleontolojia ni utafiti wa viumbe vidogo sana ambavyo huweza kuonekana kwa msaada wa darubini tu.
Dkt. Singano amekuwa mtaalamu wa kwanza wa Micropaleontolojia Afrika, akiwa ametumia sehemu kubwa ya Taaluma yake kufanya kazi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo alianzisha maabara yake mwenyewe.
“Baadhi ya tafiti ambazo tulifanya hapa Tanzania zimetumiwa na wanasayansi wengi na wasomi katika fani zao za kazi, na hadi leo, watafiti na wanasayansi wengine wa kimataifa hutumia sampuli kutoka Tanzania,” amesema Singano.
Kulingana na The Micropalaeontological Society (TMS) ambayo imempa tuzo hiyo, maarifa na mchango wa Dkt. Singano umesaidia na kutumika kwa kiasi kikubwa katika jiolojia na utafiti wa micropalaeontologia uliofanywa nchini kwa miaka ishirini iliyopita.
Hadi hivi sasa, Dkt. Singano ana machapisho 12, na amefanyiwa marejeleo 1,500.
Nishani ya Brady ni tuzo ya juu zaidi ya Jumuiya ya Micropalaeontolojia ambayo imepewa majina ya George Stewardson Brady (1832-1921) na Henry Bowman Brady (1835-1891) kwa heshima ya kutambua mchango wao katiza kuanzisha masomo ya micropaleontolojia na historia ya asili.
Medali hiyo hupewa wanasayansi ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa juu ya micropaleontolojia kupitia utafiti bora.