Uongozi wa Tabora United itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2023/24 ikitokea Championship, upo katika mpango wa kumpa ajira Kocha mzawa Fred Felix Minziro.
Klabu hiyo iliyojulikana kama Kitayosce kabla ya kupanda Ligi Kuu msimu wa 2022/23, inatajwa kuwa katika mpango huo, kufuatia Kocha Minziro kuwa huru kwa sasa, baada ya kuachana na Geita Gold FC.
Chanzo cha taarifa hizo kutoka ndani ya Uongozi wa Tabora United kimeeleza kuwa, mazungumzo ya awali baina ya pande hizo mbili yameshafanyika na Kocha Minziro amekubali ofa iliyowekwa mezani.
Chanzo hicho kimesema kuwa muda wowote kocha huyo atatangazwa kama Kocha Mkuu, hivi sasa wanakamilisha taratibu za mwisho za kumalizana.
Kimeongeza kuwa tayari kocha huyo ameanza kupewa jukumu la kusimamia usajili kimyakimya kuelekea msimu ujao wakati akisubiria kutambulishwa na uongozi wa Tabora United.
“Minziro ni suala la muda pekee kutambulishwa kuwa Kocha Mkuu mpya wa Tabora (Kitayosce) iliyopanda kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao ikitokea Championship.
“Minziro tayari amepewa mkataba ambao hivi sasa anaupitia na baada hapo ataujibu uongozi wa Tabora United na juma hili huenda akasafiri kwenda Tabora kwa ajili ya zoezi la kusaini,” kimeeleza chanzo hicho.
Alipotafutwa Minziro kuzungumzia hilo amesema kuwa: “Mimi ni kocha na kazi yangu ni kufundisha, hivyo nipo tayari kujiunga na timu yoyote itakayonipa ofa nzuri.”