MTENDAJI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametembelea Gereza la Ukonga na kukutana na viongozi wa Magereza kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali na kuimarisha ushirikiano uliopo ili kuboresha mnyororo wa utoaji haki wa wananchi.
Prof. Ole Gabriel aliwasili katika maeneo ya Gereza hilo Juni 8, 2022 majira ya saa 3.00 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Josephat Mkama ambaye aliambatana na Mkuu wa Gereza la Keko, Kamishna Msaidizi wa Magereza Rashid Mtimbe na Mkuu wa Gereza la Segerea, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamis Lissu.
Baada ya kusalimiana na viongozi hao, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alielekea ofisini kwa Mkuu wa Gereza na kupata taarifa fupi na baadaye kuzungukia maeneo kadhaa ya Gereza hilo ambapo amejionea mambo mengi na kazi nzuri za mikono zinazofanywa na wafungwa wanaotumikia vifungo mbalimbali.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Prof. Ole Gabriel ameupongeza uongozi mzima wa Magereza kwa mapokezi mazuri waliyompatia yeye pamoja na maafisa alioongozana nao na kwa fursa hiyo kwa ujumla ambapo ameahidi kuwa Mahakama ya Tanzania itafanya kila linalowezekana kutoa mchango wake ili kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
“Tumejifunza mengi, hii ni fursa nzuri ya kuona jinsi gani tunaweza kushirikiana kwa kutambua kwamba ule mnyororo wa haki una wadau wengi, wakiwemo Magereza, Polisi, Waendesha mashtaka, Mahakama na wengine. Tumeanzisha utaratibu wa kuwa na mazungumzo ya pamoja ili kubaini maeneo ambayo tunaweza kushirikiana ili Mtanzania apate haki yake kwa haraka na kwa wakati,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema kuwa jambo jingine ambalo amejifunza ni jinsi Magereza, ukiachilia mbali shughuli za utoaji haki kwa wananchi, inajishughulisha pia na uzalishaji wa vitu vingi vizuri, ikiwemo Samani ambazo ameziona na kurithika kuwa zinafaa kwa matumizi mbalimbali.
“Nisema tu kwamba sitasita hata kidogo kutumia samani zinazotengenezwa na Magereza yetu kwenye baadhi ya majengo yetu ya Mahakama mpya tunazojenga ambazo ni nyingi, hivyo hii ni moja ya fursa,” alisema.
Kuhusu kuboresha mnyororo wa haki, Prof. Ole Gabriel amewaambia viongozi hao wa Magereza kuwa Mahakama imeanzisha kituo maalumu cha Call Centre tangu Machi mosi mwaka huu kwa lengo la kupata mrejesho kutoka kwa wananchi wa huduma zinazotolewa katika maeneo mbalimbali ya kimahakama.
“Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma amekuwa akisisitiza suala la uwazi katika myororo wa haki na kupata mrejesho. Hata Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza suala la kuendelea kufuatilia ili mwenye haki na apate haki yake. Hivyo tumeamua kuanzisha call centre ambayo inafanya vizuri,” amesema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na askali Magereza.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama akabainisha kuwa kufuatia hatua hiyo Mahakama itaandaa utaratibu salama utakaowawezesha Wafungwa na Mahabusu waliopo katika magereza mbalimbali kutoa mrejesho wao kadri wanavyoona kutokana na huduma zinazotolewa na ngazi mbalimbali za Mahakama.
“Wazo hili limepokelewa vizuri na wenzetu wa Magereza, tumeweka mfumo mzuri ambao utakaowawezesha hata wananchi walipo katika Magereza waweze kutupa mrejesho ili tuone kuna nini ambacho tunaweza kuendelea kukiboresha,” alisema.
Hata hivyo, Prof. Ole Gabriel aliwakumbusha wananchi kuwa utaratibu huo ulioanzishwa sio mfumo mwingine wa kukata rufaa uamuzi uliotolewa na Mahakama, bali ni kutoa haki ya kuendelea kutoa mrejesho wa huduma zinazotolewa na Mahakama katika ngazi yoyote kuanzia Mahakama ya Mwanzo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa Magereza.
Hivyo amewasihi wananchi kokote walipo kuchangamkia fursa hiyo kwa kutumia njia rahisi za mawasiliano ikiwemo simu ya kiganjani namba 0752500400 na barua pepe ambayo ni maoni@judiciary.go.tz, huduma ambazo zinatolewa masa 24 na siku saba kwa kila wiki.
Baada ya kufanya ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alielekea katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni kuzungumza na watumishi wa Mahakama wanaofanyakazi katika Call Centre hiyo. Hakimu Mkazi Mfawishi wa Kituo hicho, Mhe. Franco Kiswaga ameahidi kushirikiana na watumishi wote ili Call Centre hiyo iweze kukidhi matarajio yaliyokusudiwa.
Katika ziara yake, Prof. Ole Gabriel aliambatana na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Victoria Nongwa, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba na viongozi wawili kutoka Call Centre, Mhe. Domician Mlashani na Bi. Evetha Mboya.