MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amemtaka mmiliki wa kiuatilifu cha salfa ya unga chapa Makonde kujisalimisha ndani ya saa 48 kutokana na tuhuma za kusambaza kiuatilifu feki kwa Wakulima.

Brigedia Jenerali Gaguti, ametoa agizo hilo ikiwa tayari watu saba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, kwa kukutwa na mifuko 2,100 ya kiuatilifu hicho waliokamatwa Wilaya za Newala na Tandahimba.

 “Watu wanne ambao ni wafanyabiashara wamekamatwa Wilaya ya Newala wakiwa na mifuko 1,600 na wengine watatu katika wilaya ya Tandahimba wakiwa na mifuko 500 sasa natoa saa 48 kwa mmiliki wa salfa chapa Makonde kujisalimisha katika mamlaka za serikali,” alisema Gaguti.

Amesema watu hao waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani baada ya utaratibu kukamilika na kutoa wito kwa Wakulima kutotumia pembejeo ambazo hazijatolewa na Serikali na kwamba wanatakiwa kutoa taarifa wakiona viuatilifu vigeni.

Kufuatia agizo hilo, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mtwara nao ukatoa wiki moja kwa mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wasambazaji wa pembejeo feki kwa Wakulima.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mtwara, Naseeb Kanduru amesema iwapo watashindwa kuchukua hatua watayaweka wazi majina ya wahusika wote wa kashifa hiyo ya pembejeo feki bila kujali nyadhifa zao.

Serikali yaitakia kila la kheri Tembo Warriors
Mtendaji Mkuu wa Mahakama atembelea Gereza la Ukonga