Klabu ya Mtibwa Sugar imeichimba mkwara Simba SC kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa 24 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaozikutanisha timu hizo Jumamosi (Machi 11).
Mchezo huo utashuhudia Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mkoani Morogoro, huku ikidhamiria kulipa kisasi cha kufungwa 5-0, kwenye mchezo wa Duru la Kwanza dhidi ya Simba SC msimu huu 2022/23.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema, kikosi chao kimekuwa na maandalizi mazuri ya kuikabili Simba SC, ambayo amekiri ina wachezaji wazuri ambao wanaweza kupata matokeo katika Uwanja wa nyumbani na ugenini.
Kifaru amesema dhamira yao kubwa ni kupata alama tatu za mchezo huo, ambazo zitawafanya kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa Duru la Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa mwaka jana 2022.
“Siku ya Jumamosi tutakuwa na Mchezo Mzuri na Mgumu katika dimba la Manungu dhidi ya Simba SC, Wachezaji wetu Wanafahamu ni Mchezo ambao tunazihitaji alama zote 3 ili tuendelee kujiweka sawa na kukaa katika nafasi nzuri “
“Tunafahamu Simba SC ina wachezaji wazuri wenye uwezo mkubwa wa kupambana katika michezo ya nyumbani na ugenini, lakini hata sisi tuna wachezaji wa kaliba hiyo, hivyo tunawakaribisha katikati ya mashamba ya miwa ili tuoneshane kazi.”
“Mbali na kuzihitaji alama tatu za mchezo huo wa Jumamosi, pia dhamira yetu nyingine ni kulipa kisasi dhidi ya wageni wetu, unakumbuka Simba SC ilitufunga mabao matano pale Dar es salaam, kwa hiyo na sisi tutahitaji kuwanyong’onyesha.” amesema Kifaru
Simba SC inakwenda mkoani Morogoro ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 54, ikitanguliwa na Young Africans iliyo kileleni kwa kumiliki alama 62.
Mtibwa Sugar ambayo ni sehemu ya timu kongwe katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ipo katika nafasi ya tisa ikiwa na alama 29, baada ya kucheza michezo 23.