Klabu ya Mtibwa Sugar imesema imedhamiria kuibuka na ushindi dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho la Tanzania Bara ‘ASFC’ utakaochezwa Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru amesema kikosi chao kipo katika maandalizi ya mwisho ya mchezo huo, huku lengo kuu ni kuondoka na ushindi ambao utawapeleka katika Hatua ya Nusu Fainali ya ‘ASFC’.
Kifaru amesema pamoja na kutambua ubora wa wanalambalamba hao wa Chamazi hawamhofii yeyote isipokuwa, Kocha Salum Mayanga amekiandaa kikosi chake kimbinu kushinda na kuingia hatua ya Nusu Fainali.
“Azam ni timu nzuri lakini haitufanyi kuwaogopa bali tunawaheshimu tukijua ubora wao. Lengo letu tunataka kushinda na kusonga mbele hatua ya Nusu Fainali na ikiwezekana kufika Fainali,” amesema.
Kifaru amesema hali za wachezaji wake ziko vizuri na kwamba wanaendelea kujiweka imara katika kambi yao ya Manungu ikiwa ni hatua za mwisho za kuelekea katika mchezo huo.
Amesema wanautaka ubingwa wa FA ili kurejea katika mashindano kama ilivyofanyika kwao mara ya mwisho 2017/2018.
Lakini huenda mchezo huo ukawa mgumu kwa kuwa hata wenyeji Azam FC baada ya kukata tamaa kwenye Ubingwa wa Ligi Kuu wanaelekeza nguvu kwenye Michuano ya ‘ASFC’ ili kusaka tiketi ya michuano ya kimataifa.
Mshindi wa mchezo huo atakutana Nusu Fainali na mshindi kati ya Simba SC dhidi ya Ihefu FC.