Wakati mamilioni ya watu Duniani wakipambana na virusi vya Corona, Imeelezwa kuwa wimbi la pili la uvamizi wa nzige linaanza tena kuyakumba mataifa ya Afrika Mashariki, safari hii likiwa na ukubwa wa karibu mara 20 zaidi ya wimbi la kwanza.
Kwamujibu wa DW , Kituo cha utabiri wa mabadiliko ya tabianchi chenye makao yake mjini Nairobi, kimesema nzige hao wanaivamia kanda ya Afrika Mashariki katika makundi makubwa kuliko ilivyowahi kushuhudiwa.
Mabilioni ya nzige hao wadogo wa jangwani wameanza kuruka kutoka kwenye maeneo yao ya viota nchini Somalia, yakitafuta majani mabichi yaliyomea baada ya mvua za msimu wa masika.
Shirika la Kilimo na chakula la umoja wa Mataifa FAO, limeutaja uvamizi wa nzige ambao kwa sehemu unasababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kuwa kitisho kikubwa kwa usalama wa chakula na maisha ya watu.