Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC leo Alhamis jioni watakua na kazi ya kuhakikisha wanachukua alama tatu muhimu mbele ya Dodoma Jiji FC ambao watakua wenyeji kwenye mchezo huo wa kiporo cha mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Simba SC wataingia dimbani wakiwa na lengo hilo, kufuatia ushindani uliopo kwenye nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu ambao unaongozwa na Young Africans wenye alama 44 baada ya kucheza michezo 18 pasina kufungwa.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakua wa kwanza Kocha Mpya wa Simba SC kwa Didier Gomes, tangu alipokubali kurithi mikoba iliyoachwa na mtangulizi wake kutoka nchini Ubelgiji Sven Vandenbroeck.
Hata hivyo tayari kocha huyo kutoka nchini Ufaransa ameshakiongoza kikosi cha Simba SC kwenye michezo ya kimataifa ya kirafiki ya ‘Simba Super Cup’, dhidi ya Al Hilal alioshinda mabao manne kwa moja, kisha kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya TP Mazembe.
Kocha huyo alipata wasaa wa kuzungumza na waandishi wa habari jana jioni na kueleza namna alivyojipanga kuwakabili Dododma Jiji FC kwenye mchezo wa leo Alhamisi.
“Utakuwa ni mchezo mgumu na wenye ushindani hasa ukizingatia kwamba kila timu inahitaji pointi tatu. Tuna mechi tatu za kucheza nazo tunahitaji ushindi hivyo haitakuwa kazi nyepesi.”
“Tuna kazi ya kupunguza pointi ambazo tumeachana na vinara wa Ligi Kuu Bara ambao ni Young Africans.”
Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 35 baada ya kucheza michezo 15 inakutana na Dodoma Jiji ambayo ipo nafasi ya 10 na alama zake 22.