Wazazi wawili wamejikuta katika hali ya kuchanganyikiwa mara baada ya mtoto wao kutangaza azma yake ya kuwapeleka mahakamani na kuwafungulia mashtaka kwa kosa la kumzaa bila idhini yake.
Raphael Samuel, mwenye umri wa miaka 27, ambaye ni raia wa India, amesema kuwa yalikuwa makosa makubwa kwa wazazi wake kumzaa bila ya idhini ya moja kwa moja kutoka kwake.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Kanak la nchini India, Samwel amesema kuwa ingawa anafahamu kwamba haiwezekani kwa mtu kupeana idhini ya kuzaliwa, anashangaa ni kwa nini watu huzaliwa bila idhini yao kueleza azma au nia ya kuishi maisha hapa duniani.
Aidha, Samwel ameongeza kuwa anawasiliana kwa karibu sana na mawakili wake ambapo amesema kuwa hivi karibuni watawasilisha kesi hiyo kwa msingi kwamba hafai kuendelea kupata mateso anyoyapitia hapa duniani kwa sababu haukuwa uamuzi wake kuzaliwa.
Hata hivyo, Watu wengi wanahofu kuwa suala hilo linaweza kuleta mtafaruku katika jamii, lakini wazazi wa Samuel, ambao wote wawili ni mawakili, hawana wasiwasi wowote kuhusu hatua hiyo ya mtoto wao kutaka kuwashtaki mahakamani kwa kosa la kumzaa bila idhini yake.