Mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda, Osama Bin Laden ametoa vitisho vipya kwa nchi za Magharibi akiwataka kutarajia mashambulizi ya kulipa kisasi.
Hayo yamesemwa na afisa wa FBI, Ali Soufan aliyeongoza upelelezi dhidi ya kundi hilo la kigaidi hususan kupekuwa nyaraka zilizokutwa kwenye nyumba aliyouawa Bin Laden nchini Pakistan.
Kupitia mahojiano aliyofanya na shirika la habari la CBS, Soufan alisema kuwa mtoto huyo wa Osama anayefahamika kwa jina la Hamza Bin Laden ambaye sasa hivi ana umri wa miaka 28, ametoa vitisho hivyo kwa njia na maneno yenayofanana na yaliyokuwa yakitumiwa na baba yake.
“Ujumbe wake wa hivi karibuni… alitoa hotuba kama vile ni baba yake ndiye aliyekuwa anatoa hotuba ile, akitumia sentensi, na istilahi ambazo zilikuwa zikitumiwa na Osama bin Laden,” alisema Soufan.
“Kwa ufupi alisema, ‘Watu wa marekani, tunakuja na mtaipata hisia. Na tutalipa kisasi cha kifo cha baba yangu, Iraq na Afghanistan,” aliongeza.
Afisa huyo wa FBI alisema kuwa Hamza anaandaliwa kuwa kiongozi wa kundi hilo na kwamba anaonesha kuwa na uwezo unaofanana na baba yake kiasi cha kulishawishi kundi hilo.
Tangu mwezi Januari mwaka huu, Hamza aliongezwa rasmi kwenye orodha ya magaidi wanaotafutwa zaidi na Marekani.
Akiwa na umri wa miaka 22, Hamza amedaiwa kuwa aliandika barua kwa baba yake ambaye hajawahi kumuona kwa miaka kadhaa baada ya kuua. Soufan alitaja sehemu ya barua hiyo kuwa “Nakumbuka kila muonekano…. Kila tabasamu ulilonipa, kila neno uliloniambia.”
Makomando wa kikosi maalum cha jeshi la Marekani waliendesha oparesheni maalum iliyofanikisha kumuua Osama Bin Laden nchini Pakistan mwaka 2011, ikiwa ni karibu muongo mmoja tangu alipotengeneza na kuhuisha shambulizi la kigaidi nchini Marekani la Septemba 11.