Vyombo vya usalama nchini Ufaransa vimeanzisha uchunguzi wa kina kumsaka mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, baada ya chombo cha habari za uchunguzi kuweka hadharani picha yake akiwa nchini humo.
Kamera za Mediaapart zilimnasa Aloys Ntiwiragabo akiwa katika maeneo ya mji wa Orleans, kilometa 100 kutoka jiji la Paris, baada ya vyombo vya usalama vya kimataifa kushindwa kumpata kwa miaka mingi.
Ntiwiragabo aliyekuwa mwanajeshi wa jeshi la Rwanda wakati huo, alitajwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) kuwa ni mmoja kati ya watu waliotengeneza mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, yaliyosababisha vifo vya watu takribani 800,000.
ICTR, Rwanda na Ufaransa walikuwa wamepunguza nguvu ya kumtafuta, lakini picha za video na mgando zilizowekwa mtandaoni na ‘Mediaapart’ zimewafanya waanze tena msako kwa nguvu zaidi.